Highlights

MSICHANA ANAYETAMBUA THAMANI YAKE



Thamani yako ni jinsi ambavyo wewe binti ulivyo,umeumbwa kwa namna ya tofauti sana na ya ajabu. Kama ulikuwa haujui naomba uwe unajua hilo, kuwa wewe ni wa thamani kuanzia sura yako jinsi ilivyo, ingawa unajikosoa sana na kumwona mwenzako ndiye bora kuliko wewe. Ngozi yako ni nzuri hauhitaji kuji ‘cream’,sauti yako ni ya tofauti na ndiyo inayokuwakilisha wewe kama wewe na sio binti mwingine, umbile yako ni la tofauti na huyo ndiye wewe na sio mtu mwingine na hautakaa uwe mtu mwingine. Utakuwa wewe daima na ndilo kusudi la kuumbwa kwako.

Binti wewe ni wa thamani kubwa sana mbele za Mungu na mwili wako ni wa thamani sana.Haijalishi wewe unajionaje au wenzako wanakuonaje pia, ila kuna namna Mungu anavyokuona ambavyo ni tofauti kabisa na jinsi watu wanavyokuona. Mbele ya Macho ya Mungu wote ni wa thamani sana hakuna kupanda thamani au kushushwa thamani na Mungu , wanadamu wanaweza kufanya hivyo ila sio kwa Mungu wetu thamani yetu kwake iko pale pale .Hebu ona jinsi Mungu anavyosema juu yako katika Isaya 49; 16“Tazama nimekuchora katika vitanga vya mikono yangu na kuta zako ziko mbele zangu daima”.Haijalishi wewe unajionaje ndani yako au wazazi wako wanakuchukuliaje au mazingira uliyopo yanakuchukuliaje lakini muda huu unaposoma hapa natamani uone jinsi Mungu anavyokuona yeye, ni tofauti kabisa na wazazi wanavyokuona, tofauti na marafiki wanavyokuona ni tofauti na ‘boy friend’ ambaye ulilala naye na amekuacha anavyokuona, ni tofauti na yule mume wa mtu uliyekuwa naye kwenye mahusiano, ipo namna ambayo Mungu anakuona amesema AMEKUCHORA. Kuchorwa ni kitu cha pekee na cha thamani kubwa mbele za Mungu.

 Mungu anakufahamu na anakupenda kuliko yeyote yule. Wakati mwingine wazazi wanaweza kutusahau au kutuacha, lakini Mungu anajua thamani yako na ni yeye pekee anayejua kusudi la kuumba wewe.
 Jikubali jinsi ulivyoumbwa, jikubali na jivunie kuumbwa msichana. Kuna mabinti hawafurahii kuumbwa kwao wasichana na wengine wanajinenea ni bora wangekuwa wanaume, hii sio sahihi kabisa,Mungu alijua kuwa unafaa kuwa msichana na akakuumba hivyo ulivyo ili akutumie kulifanya lile yeye alilokusudia katika maisha yako. Kama ulikuwa unanung’unika kuumbwa msichana kwa sababu kila mwezi unaingia periods, wengine hawapendi sehemu za miili yao mfano; Maziwa, makalio, miguu n.k sasa ni wakati wako wa kujitambua na kujikubali namna Mungu alivyokuumba na kutubu pale ulipomkosoa Mungu, kwani Mungu huwa hakosei daima. Hivyo na kwa jinsi umbo lako lilivyo, Mungu ameweka hazina ya ajabu ndani yako wewe binti.

Usiibadilishe thamani yako kwa kujifanya mwanaume, kuna ndoa za jinsia moja ambazo mabinti kwa mabinti wanaoana ambapo ni kinyume na makusudio ya Mungu kukuumba wewe. Jikubali na jithamini na upende mwili ambao Mungu amekupa ana kusudi lake maalum la kukupa mwili huo.




No comments